HIZI HAPA SABABU ZA KUSHUKA KWA MFUMUKO WA BEI KWA MWEZI OKTOBA
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa
mwezi Oktoba, 2017 umepungua hadi kufikia asilimia 5.1 ikilinganishwa na
asilimia 5.3 ilivyokuwa mwezi Septemba, 2017.
Akizungumza na Waandishi wa Habari
leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu Irenius Ruyobya wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) amesema kupungua kwa Mfumuko wa Bei
kunamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka
ulioishia Oktoba, 2017 imepungua ikilinganishwa na kasi ilivyokuwa kwa mwaka
ulioishia Septemba, 2017.
Ruyobya ameongeza kuwa, kupungua
kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Oktoba, 2017 kumechangiwa na kupungua kwa bei za
baadhi ya bidhaa za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Oktoba, 2017
zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba, 2016.
"Baadhi ya bidhaa za
vyakula zilizochangia kupungua kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja na unga wa mtama kwa asilimia 2.6,
samaki kwa asilimia 7.1, matunda kwa asilimia 2.7, mbogamboga kwa asilimia 7.4,
maharage kwa asilimia 2.9, viazi kwa asilimia 14.4 na karanga kwa asilimia
7.8", amesema Ruyobya.
Akizungumzia Mfumuko wa Bei kwa
upande wa Afrika Mashariki, Irenius Ruyobya amesema Mfumuko wa Bei wa Tanzania
una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo
nchini Kenya Mfumuko wa Bei wa mwezi Oktoba, 2017 umepungua hadi asilimia 5.72
kutoka asilimia 7.06 mwezi Septemba, 2017 na nchini Uganda umepungua hadi
asilimia 4.8 mwezi Oktoba, 2017 kutoka asilimia 5.3 mwezi Septemba, 2017.
Mfumuko wa Bei wa Taifa unapima
kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na
kaya binafsi nchini.
Post a Comment