UWANJA WA NDEGE DODOMA KUTUMIKA MASAA 24
Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi wa kufunga Taa za kuongozea ndege ili kuruhusu Uwanja wa Ndege wa Dodoma kuweza kutumika masaa 24.
Akizungumza hayo mjini Dodoma
mara baada ya kukagua Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light)
zilizofungwa uwanjani hapo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa hatua hiyo ni muendelezo wa
uboreshaji wa uwanja huo katika kuruhusu ndege za aina zote kutua masaa
24 kwa wiki.
“Hii ni hatua ya pili ya
uboreshaji wa uwanja huu ambapo hatua ya kwanza tumeimaliza ya upanuzi
wa barabara za kuruka na kutua ndege (runway) hadi kufikia KM 2.5”,
amesema Waziri Profesa Mbarawa.
Aidha, ameongeza kuwa ufungaji wa
taa hizo umegawanywa kwa hatua tatu ambapo awamu ya kwanza imekamilika
kwa kujumuisha ufungaji wa Mfumo wa Kisasa wa Taa za Umeme Jua (Aviation
Solar Powered Light), katika barabara za kuruka na kutua ndege na
maeneo ya maegesho, hatua ya pili ni kufunga taa za kumsaidia Rubani
kuweza kuona uwanja wote na hatua ya mwisho ni taa zitakazofungwa mita
400 kila upande uwanjani hapo.
Amefafanua kuwa Taa hizo za
kisasa (Aviation Solar Powered Light) zitapunguza gharama za uendeshaji
uwanjani hapo ikiwemo matengenezo yake kwani zinadumu muda mrefu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
Wizara, Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho, amesema kuwa nia ya
Serikali ni kuendelea kurefusha uwanja huo ambapo italipa fidia kwa
nyumba zilizopo pembeni ya uwanja huo ili kuongeza usalama wa uwanja na
ndege kwa ujumla.
“Tutaweka uzio katika uwanja huu
kulingana na matakwa ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na pia kupitia uzio
huu taa zitakuwa salama”, amesisitiza Dkt. Chamuriho.
Naye, Msimamizi wa mradi Bw.
Samwel Mruma kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), amesema
mfumo wa taa hizo za kisasa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light),
zimefungwa kwa siku 14 na zina uwezo wa kufanya kazi kwa miaka 12 na
kuwaka kwa masaa laki moja ukilinganisha na nyingine ambazo zinawaka kwa
masaa elfu kumi.
Mfumo wa uwekaji Taa za Kisasa ni
mkakati wa Serikali katika kuhakikisha inaendelea kuboresha viwanja
vyake vya ndege ili kukidhi viwango vianavyostahili katika usafiri wa
anga.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia), akitoa maelekezo kwa
Msimamizi wa mradi Bw. Samwel Mruma kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Nchini (TAA), wakati alipokagua mfumo wa Kisasa wa Taa za Umeme Jua
(Aviation Solar Powered Light), zilizofungwa katika Uwanja wa Ndege wa
Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara, Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard
Chamuriho na kulia ni Meneja wa Uwanja huo Julius Mlungwana.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akionesha kifaa (Remote Controller)
cha kuwashia Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light),
zilizofungwa katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa waandishi wa habari,
wakati akikagua Taa hizo uwanjani hapo.
Muonekano wa Mfumo wa Kisasa wa
Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), zilizofungwa katika
Uwanja wa Ndege wa Dodoma. Taa hizo zitatumika kuongozea ndege nyakati
za Usiku na zina uwezo wa kuwaka masaa laki moja.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), akitoa maelekezo kwa Katibu
Mkuu wa Wizara, Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho (katikati), na
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Leonard Chimagu
(kushoto), wakati alipokagua mfumo wa kisasa wa Taa za Umeme Jua
(Aviation Solar Powered Light), katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma.
………………………………………………………..
Post a Comment