WAZIRI UMMY AMUAGIZA RMO WA RUKWA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA KATIKA NGAZI ZOTE ILI KUTEKELEZA SERA YA AFYA
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kuboresha huduma za afya katika ngazi zote ili kuwasaidia wananchi wa mkoa huo kulingana na sera ya afya.
Hayo ameyasema leo wakati wa ziara yake ya kukagua huduma za Afya katika Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa.
“Maelekezo yangu tujenge hospitali zetu za Wilaya kwa sababu pia idadi ya watu inazidi kuongezeka hivyo zitasaidiana na zile za taasisi zisizo za kiserikali ili kutimiza sera na miongozo ya Serikali”
Aidha, Waziri Ummy amemtaka Mganga Mkuu huyo kufuatilia kwa ukaribu huduma zitolewazo na hospitali za taasisi zisizo za kiserikali ili kuhakikisha kwamba zinafuata miongozo na sera ya Afya
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasulu amesema kuwa wanazo changamoto mbali mbali zinazoikumba Mkoa wake zikiwemo upungufu wa watumishi wa Afya kwani Mkoa unahitaji jumla ya watumishi 3489 lakini waliopo ni watumishi 1593 sawa na 46% huku kukiwa na upungufu wa watumishi 1895 ambayo ni sawa na 54%.
Aidha ,Dkt. Kasulu amesema kuwa licha ya changamoto zilizopo ameipongeza Serikali ya awamu ya Tano kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na ushirikiano na wadau mbalimbali kwa kuwajengea vyumba vya upasuaji katika vituo tisa huku vituo sita vikiwa vinamilikiwa na Serikali jambo linalosaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Mbali na hayo Dkt. Kasulu amemshukuru Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe magufuli kwa kuwapatia magari mawili ya kubebea wagonjwa jambo ambalo limesaidia kupunguza hadha ya hospitali nyingi ikiwemo vifo vya mama wajawazito.
Post a Comment