WALICHOAMBIWA LEO WALIOPATIWA MAFUNZO YA MIONZI
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Hussen Laisser akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunga mafunzo ya siku tano yaliyohusu udhibiti wa mionzi yaliyofanyika kwenye hoteli ya New Afrika jijini Dar es salaam na kuhudhuria na maofisa wa Interpool kutoka nchi za Afrika Mashariki, Kati na na Kusini mwa Afrika.
……………………………………………………………………
Na Neema Mathias na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wadau wa masuala ya mionzi wameaswa kufanyia kazi maarifa na ujuzi waliopata katika semina ya siku 5 ya namna ya kufahamu na kudhibiti vyanzo vya mionzi.
Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Hussen Laisser alipokuwa akifunga mafunzo hayo ambayo kwa mara ya kwanza yamefanyika nchini.
DCP Laisser amesema kuwa mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Wizara ya Nishati ya Marekani na Sekretari ya Interpol ya nchini Ufaransa yalihusisha jumla ya wadau wa masuala ya mionzi 59 kutoka katika nchi tisa zikiwemo za Botswana, Afrika Kusini, Malawi, Ethiopia, Kenya, Mauritius, Tanzania pamoja na Zambia.
“Vyeti mlivyotunukiwa leo vimewatambua kama wawakilishi wa wengi waliobaki katika nchi zenu hivyo mnaporudi katika nchi zenu msitumie vyeti hivyo kama mapambo bali mtumie ujuzi mlioupata kuwaelimisha na wengine,” alisema DCP Laisser.
DCP Laisser ameongeza kuwa mionzi ina manufaa kwa jamii lakini isipotumika au kutunzwa vizuri inaleta madhara hivyo mafunzo hayo yamelenga kuwaandaa wadau mbalimbali wa masuala hayo kufahamu namna ya kugundua, kuchunguza na kudhibiti mionzi.
Aidha, DCP Laisser amewatoa hofu Watanzania kuwa hakuna uhalifu unaotokana na mionzi lakini lengo la mafunzo hayo ni kujiandaa kupambana na matukio ya kiuhalifu ambayo yanaweza kutokea.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Teknolojia ya Mionzi, Dkt. Firmi Banzi amesema kuwa sababu kubwa ya kukosekana kwa mafunzo ya masuala ya mionzi kwa Tanzania ni ukosefu wa wataalam na vifaa kwani vifaa hivyo vina gharama kubwa.
“Kwa kuwa mionzi haiwezi kugundulika kwa kutazamwa, kunuswa au kuguswa bali huitaji vifaa maalum hivyo tunawashukuru wafadhili wa mafunzo haya kwa sababu baada ya mafunzo wanatukabidhi vifaa vitakavyotumika kutambua mionzi,” alisema Dkt. Banzi.
Mafunzo hayo yamefanyika mara sita katika nchi tofauti tofauti, kwa Tanzania ni mara ya kwanza mafunzo hayo kufanyika.
Post a Comment