RAIS DKT,MAGUFULI APONGEZWA KWA UPATANISHI
Na Judith Mhina – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli amepongezwa na viongozi wa Dini 170 kutoka Tanzania na Kenya katika suala zima la upatanishi.
Pongezi hizo zimetokana na kitendo cha Rais kuwapatanisha Mkuu wa Mkoa Dar-es-Salaam, Mhe. Paul Makonda na mmiliki wa Kituo cha Televisheni na Redio cha Clouds Bw, Ruge Mutahabwa, kuwa ni kielelezo cha kuigwa na Wakenya mara baada ya kukamilika kwa uchaguzi wao.
Akiongoza maombi hayo maalum, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili na Amani kwa Maaskofu na Maashekhe nchini Tanzania Askofu William Mwamalanga na viongozi wa Dini wa kutoka Kenya na Tanzania, walipiga kambi ya kuombea uchaguzi Mkuu nchini Kenya kwa muda wa mwezi mmoja Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar-es-Salaam.
Akifunga maombi hayo na kuwaaga viongozi wa dini na vijana kutoka Kenya Askofu William Mwamalanga amesema; Kitendo cha Rais John Magufuli kumpatanisha Ruge Mutahabwa na Paulo Makonda ni cha kishujaa na muhimu kuigwa na Kenya ili wapatane kwa kuwa uchaguzi umekwisha, haingii akilini kuendelea na maisha ya chuki ugomvi na malumbano ambayo yaweza kuleta utengano.
Akiwasihi kwa msisistizo washiriki kutoka Kenya amesema; “Nendeni Kenya mkawe wapatanishi wa kweli mwambieni Mheshimiwa Raila Odinga na wote ambao wamekosa uongozi katika uchaguzi huo, waridhie matokeo na kujumuika kama raia wema kuijenga Kenya mpya.
Akisisitiza jambo hilo, Askofu ameomba watu wote Kenya wajipatanishe nafsi zao na MUNGU ili kuijenga kenya kwa ajili ya ustawi wa wakenya wote bila ubaguzi.
Katika kuthibitisha upatanishi uliofanywa na Rais Magufuli, Askofu Mwamalanga alipiga simu kwa Bw, Ruge ambaye amesema; “Nimefurahishwa sana na hatua ya Rais Magufuli ya kutupatanisha, nimepokea kwa’ furaha hakika ni kazi njema ambayo inatakiwa kuungwa mkono na jamii yote. Hakuna sababu kuishi kwa chuki zisizo na maana, naomba niwashukuru Maaskofu kwa kunipongeza”.
Naye Shekhe Abrahamani Mohamed aliyeshiriki ibada hiyo amesema; “Bw, Ruge Mutahabwa ni mtu aliyekomaa kisiasa, ana hekima, na mwenye upeo mkubwa wa fikra. Hivyo nawasihi vijana wa Tanzania na Kenya kuiga mfano huo maana haipendezi kuishi kwenye maisha ya chuki”.
Chuki ni kikwazo cha maendeleo tunaomba upatanisho wa Rais Magufuli uendelee kwa watu wengine wanaishi na maisha ya kuchukiana na sisi viongozi wa kiroho tuwe mfano wa kupatana wenyewe”. Amesema Shekhe Abrahamani.
Maombi hayo na Dua yaliongozwa na Askofu Mwamalanga na kuhudhuriwa na vijana 400 wakristo kutoka Vyuo vikuu vya Tanzania na wanawake 283, kutoka Kenya, na wanawake 500 kutoka Tanzania. Aidha, kulikuwa na washiriki wake kwa waume kutoka Marekani 3 Uingereza, 5 Malawi, 6, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 15, Zambia 7, Uganda 2 na Israel 2.
Maombi hayo yalimalizika kwa kurejea kitabu cha Mathayo 5 msatari wa 9 nanukuu; “Heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki maana ufalme wa mbinguni ni wao”.
Post a Comment