WANAODAIWA NA BODI YA MIKOPO WATAKIWA KULIPA MADENI YAO
Bodi ya mikopo ya Elimu ya Juu nchini imewataka wanaodaiwa
na Bodi hiyo kurejesha mikopo yao ili na wengine waweze kukopa badala ya
kusubiri kuchukuliwa hatua.
Akiongea katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na
Televisheni ya Taifa (TBC) Mkurugenzi wa Bodi ya mikopo ya Elimu ya Juu
Abdul Badru alisema tangu waanze mfumo wa kuwabana wadaiwa kupitia
waajiri wao kasi ya urejeshwaji mikopo imeongezeka.
Alisema pamoja na kuwabana pia wamekuwa wakitoa elimu
kuhusu umuhimu wa kurejesha mikopo hiyo pamoja na kutunga sheria ya
kuwabana wasiolipa mikopo.
Awali kabla ya kuwekwa kwa msukumo katika kudai mikopo hiyo
urejeshwaji ulikuwa wastani wa shilingi bilioni 5 mpaka 6 kwa mwezi
lakini kwa sasa wanapata marejesho ya mikopo zaidi ya Bilioni 10.
Bw. Badru alisema hivi sasa wameboresha mfumo wa utoaji
mikopo kwa kuziba mianya ya wanafunzi hewa pamoja na wale wasiokuwa na
sifa ambao wamekuwa wakipeleka vielelezo vya uongo.
Alisema licha ya kupitishwa kwa orodha ya wanafunzi
wanaostahili mikopo uhakiki umekuwa ukifanyika kila baada ya miezi
mitatu ambapo maofisa wa bodi hiyo huenda vyuoni ili kujiridhisha kama
wanafunzi waliolengwa kwenye mikopo hiyo wapo.
“Kwa mfano mwaka jana wanafunzi elfu tatu miongoni mwa
walioomba mikopo kwa madai ya kufiwa na wazazi waliwasilisha vyeti vya
Vifo vya wazazi wao ambavyo baada ya kupelekwa RITA walishindwa
kuvitambua”Alisema BADRU.
Alisema mwanafunzi anayekosa mkopo kama anavyo vigezo vyote
vinavyotakiwa hutakiwa kukata rufaa ili ufanyike upitiaji upya wa
nyaraka zake.
Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya shilingi Bilioni 483
zimetengwa kwaajili ya kuwakopesha wanafunzi 120,000 kutoka vyuo tofauti
nchini.
Post a Comment