MITUMBA SASA BASI "MAJALIWA"
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akingalia mitambo ya kutengeneza Nguo katika Kiwanda cha NIDA kilichopo Jijini Dar es salaam. Waziri Mkuu alifanya ziara katika kiwanda hicho Jumamosi 15 july 2017 kushoto anaye toa maelezo ni Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha kutengeneza Nguo cha NIDA Bwana Muhammadhamza Rafiki na kushoto ni Meneja Mkuu wa Kiwanda cha NIDA Bwana Muhammad Waseem
,Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katikati akionyeshwa Ubora wa Kanga zinazo tengenezwa hapa nchini katika kiwanda cha NIDA wakati alipofanya ziara Jumamosi 15 july 2017 katika kiwanda hicho kilichopo Jijini Dar es salaam wanao muonyesha kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha kutengeneza Nguo cha NIDA Bwana Muhammadhamza Rafiki na kushoto ni Meneja Mkuu wa Kiwanda cha NIDA Bwana Muhammad Waseem
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
……………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema safari ya Watanzania kuachana na nguo za mitumba imewadia kutokana na uwepo wa viwanda vya kutengeneza nguo nchini.
Pia amesema uwepo wa viwanda hivyo utasaidia wakulima wa pamba kupata soko la uhakika hivyo amewataka walime pamba ya kutosha ili viwanda vipate malighafi.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Julai 15, 2017) wakati alipotembelea kiwanda cha nyuzi cha Namera kilichoko Gongo la Mboto na kiwanda cha nguo cha Nida kilichopo Ubungo Dar Es Salaam.
Alisema viwanda vya kutengeneza nguo nchini ni ushahidi tosha kwamba nchi iko njiani kuondokana na matumizi ya nguo za mitumba kwa kuwa nguo nyingi zitakuwa zinatengenezwa nchini, hivyo kupatikana kwa bei nafuu.
Alisema kwa sasa wanunuzi wa pamba hawana sababu ya kwenda kuuza nje ya nchi na badala yake wauze katika viwanda vya ndani ili vizalishe nguo za kutosha zitakazouzwa nchini kwa gharama nafuu.
“Pamba yote inaweza kuchakatwa nchini, hivyo hakuna haja ya kuiuza nje ya nchi. Natoa wito kwa wakulima wetu wa pamba walime mazao ya kutosha kwa sababu soko la uhakika ipo na hii ndio safari ya mwisho ya mitumba.”
Awali Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha saruji cha Lake kinachozalisha saruji ya nyati ambapo aliwapongeza wawekezaji wote nchini kwa kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. John Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda.
Katika kiwanda hicho ambacho kinazalisha tani 700,000 kwa mwaka kimeajiri watu 2000 na kinalipa kodi ya sh. bilioni 81.312 kwa mwaka, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wake wawe waaminifu, wafanye kazi kwa weledi na wawe waadilifu.
Pia Waziti Mkuu alitoa wito kwa wamiliki wa viwanda vyote nchini kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi waishio katika maeneo ya karibu na viwanda sambamba na kulipa kodi kwa wakati na kwa viwango sahihi.
Post a Comment