SERIKALI YALAANI KITENDO CHA KUUMIZWA KWA WANAHABARI
UMUHIMU WA JAMII KULINDA HAKI NA USALAMA WA WANAHABARI
Dodoma, Jumatatu, April 24, 2017:
Serikali imepokea kwa masikitiko taarifa za kushambuliwa
na kujeruhiwa baadhi ya waandishi wa habari katika mvutano uliotokea
juzi jijini Dar es Salaam kati ya wafuasi wa pande mbili zinazokinzana
za Chama cha Wananchi (CUF). Tumechukua muda kidogo kulifuatilia suala
hili na kubaini licha ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti polisi, wapo
waandishi ambao vifaa vyao vya kazi pia vililengwa katika shambulizi
hilo.
Tunachukua fursa hii kulaani kitendo cha kuumizwa
wanahabari tena waliokuwa wamealikwa kuhudhuria mkutano huo. Ifahamike
kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa
kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande
zinazofarakana katika jamii.
Kifungu cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.
12 ya mwaka 2016 kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya
habari kwa muktadha wa kuwepo katika maeneo ya matukio kama hakuna
sababu nyingine za kuzuiwa. Misingi ya uhuru huu wa kitaaluma pia
imesisitizwa katika Ibara za 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na
Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu imeuridhia.
Tunawatakia nafuu ya haraka wanahabari waliojeruhiwa na
wenzao wengine waliopatwa na jakamoyo katika tukio hilo. Kwa kuwa suala
hili tayari limeripotiwa polisi, tunawaomba wadau wote wa habari na
wanasiasa kwa sasa kutulia na kuviachia vyombo husika vilifanyiekazi ili
hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali
Post a Comment