Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli ameamua
madaktari 258 na wataalamu wa Afya 11 walioleta maombi na kukidhi vigezo
kupitia Wizara ya Afya kwa ajili ya kwenda kufanya kazi nchini Kenya
kuajiriwa na Serikali.
Hayo
yamebainishwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari
katika Viwanja vya Bunge Mjini Dodoma.
“Kwa
upande wetu sisi ratiba ya utekelezaji wa ajira hizi za madaktari hao
ilikubalika na pande zote iwe tarehe 6 Aprili 2017 na Madaktari hao wawe
tayari kusafiri kwenda nchini Kenya kati ya tarehe 6-10 Aprili 2017,
hadi tarehe ya Taarifa hii Mahakama nchini Kenya haijaondoa pingamizi
lililofunguliwa kuhusu Ajira za madaktari wa Tanzania nchini
Kenya,”Alisisitiza Mhe.Mwalimu.
Amesema
kufuatia uamuzi huu majina ya Madaktari husika na vituo
watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika Tovuti ya Wizara pamoja na
wataalamu wengine wa afya 11 walioleta maombi yao na kukidhi vigezo.
Aidha
Serikali ya Tanzania itakuwa tayari kushughulikia upya ombi la Serikali
ya Kenya kupatiwa Madaktari 500, pale ambapo hakutakuwa na vikwazo vya
kupeleka madaktari wetu nchini Kenya.
Mnamo
tarehe 18 Machi 2017 Ujumbe wa Serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri
wa Afya Dkt.Cleopa Mailu uliwasili nchini ambapo ulikutana na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli kwa madhumuni ya
kuomba kuajiri kwa Mkataba Madaktari wa Tanzania mia tano(500) ili
kupunguza uhaba wa Madaktari nchini Kenya na kukubali ombi hilo.
Aidha
Maombi hayo yalipokelewa ambapo jumla ya maombi 496 yaliwasilishwa na
baada ya kufanya uchambuzi wa maombi hayo ilibainika kuwa Madaktari 258
walikidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanya kazi nchini Kenya,lakini
wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea kukamilisha utaratibu wa ajira za
Madaktari hao Madaktari watano wa Kenya waliwasilisha pingamizi
mahakamani kuitaka Serikali ya nchi yao kusitisha kuajiri Madaktari
kutoka Tanzania.
Post a Comment