POMBE,MIKATE VYAGOMBANIWA MOSHI
Mikate
jana asubuhi iligeuka bidhaa adimu katika maduka makubwa mjini Moshi,
kutokana na wingi wa wateja uliosababishwa na utamaduni wa wenyeji wa
Mkoa wa Kilimanjaro kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka
walikozaliwa.
Mbali
ya wingi wa wageni waliorejea kusherehekea sikukuu, msongamano wa
magari katikati ya mji na barabara ya njia panda ya Himo-Moshi jioni
unaonekana kuvunja rekodi.
Maduka
makubwa ya bidhaa (supermarkets), jana asubuhi yalikuwa hayana mikate
kutokana na mingi kununuliwa juzi na wenyeji wanaoenda vijijini kwa
ajili ya sikukuu.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti la Mwananchi kati ya saa mbili asubuhi hadi saa
nne uliobaini upungufu wa mikate na wasambazaji walichelewa kuisambaza.
Katika baadhi ya maeneo mikate iliyokuwepo ni iliyokaa dukani kwa zaidi ya siku mbili.
“Hatuna
kabisa mikate, ilimalizika jana (juzi) usiku kwenye saa tatu. Wateja
walikuwa wengi na kila mmoja alinunua mkate mmoja au miwili kwa ajili ya
kwenda nayo kijijini,” alisema mhudumu mmoja.
Katika maduka hayo, bidhaa nyingine iliyonunuliwa kwa wingi ni bia na pombe kali.
Vilevile
kulikuwa na misururu mirefu ya wateja wakinunua bidhaa hizo na kupakia
kwenye magari. Wateja pia walikuwa wengi kwenye masoko ya Mbuyuni na
Kati.
Mji wa Moshi kwa siku tatu mfululizo hadi jana umeonekana kuelemewa na wingi wa magari.
Barabara
Kuu ya Dar es Salaam -Moshi, ndiyo iliyotia fora kwa msongamano wa
magari kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa tatu usiku. Nyingine
iliyokuwa na msongamano ni ya kutoka stendi kuu hadi mzunguko wa magari
wa YMCA.
Kutokana
na msongamano huo, magari yalikuwa yakitumia hadi dakika 40 kutoka eneo
la Stop and Shop karibu na Kiboriloni hadi katikati ya mji, wakati kwa
siku za kawaida huchukua kati ya dakika tatu hadi tano.
Msongamano
pia ulikuwepo barabara lilipo Kanisa Katoliki la Kristo Mfalme hadi
masoko ya Mbuyuni na Kati na barabara ya kuelekea Arusha.
Askari
wa usalama barabarani wamejikuta katika wakati mgumu wa kuongoza magari
kuanzia barabara ya Polisi Majengo, mzunguko wa magari wa YMCA na soko
la Mbuyuni.
Gazeti
la Mwananchi lilishuhudia waendesha pikipiki maarufu bodaboda
wakihusika katika ajali wengi kwa kugonga magari kwa nyuma ikidaiwa hilo
linachangiwa na kutokuwa wazoefu wa foleni kama ilivyo jijini Dar es
Salaam.
Mmoja
wa wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro anayeishi Dar es Salaam ambaye jana
alikuwa kijijini kwao Mwika, Moshi Vijijini, William Shao alisema kwa
sasa kinachoendelea ni masuala ya kunywa na kula.
“Huku
ni sherehe tu tunakula na kunywa, tena kuna ile Mbege (pombe ya asili
kwa Wachaga) original (halisi) kabisa. Ni ndafu, mbege na kula. Huu ni
utamaduni mzuri sana,” alisema Shao.
Na Daniel Mjema, Mwananchi
Post a Comment