Header Ads

header ad

HUU HAPA WITO KWA VYUO VIKUU NCHINI



Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha amevitaka Vyuo Vikuu kuzingatia miongozo inayotolewa katika uanzishaji wa programu, udahili wa wanafunzi, ajira za wahadhiri na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. 

Naibu Waziri ametoa agizo hilo katika mahafali ya 10 ya Chuo Kikuu cha Mt. Joseph Tanzania (Sjuit) yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho Mbezi Luguruni Dar Es Salaam leo, ambapo amesema Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) vihakikishe  taratibu zote, kanuni na sheria za ithibati zinazingatiwa ili kukidhi matakwa ya viwango vya Elimu ya Juu nchini.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema katika kuhakikisha ubora wa Elimu inayotolewa na Vyuo na Taasisi za Elimu ya Juu nchini, Serikali kupitia tume ya Vyuo Vikuu Tanzania imeboresha kanuni na taratibu za miundo na uanzishaji wa mitaala ya Vyuo Vikuu kwa kuzingatia Tuzo za Vyuo Vikuu (Universities Qualifications Framework - UQF). Vilevile, Serikali kupitia TCU inaendela na maandalizi ya Mfumo wa Uthibiti Ubora kwa vyuo vyote (Quality Assurance Framework)

Mheshimiwa Ole Nasha amesema katika kuthibiti Ubora wa Elimu inayotolewa katika Vyuo, Serikali iliendesha zoezi la uhakiki katika Vyuo mbalimbali ili kubaini uwezo wa vyuo katika uendeshaji wa mafunzo, ambapo Vyuo Vikuu 05, Vyuo Vikuu Vishiriki 10 na Vituo 04 vilifungiwa kwa kutokidhi viwango vya ubora kulingana na miongozo ya TCU na NACTE mpaka pale usajili utakapofanyika upya. 

Aidha, Naibu Waziri ameeleza kuwa programu 46 katika vyuo 13 zilibainika kuendeshwa bila ithibati na kuendeshwa kinyume cha sharia jambo ambalo lilipelekea Serikali kusimamisha udahili kwa program hizo mpaka zitakapopata ithibati kutoka mamlaka husika.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Burton Mwamila amesema katika kuhakikisha chuo kinakidhi matakwa ya sheria ya vyuo Vikuu na kanuni zake uongozi wa  Juu wa Chuo umebadilishwa, miundombinu ya ufundishaji na kujifunzia,  sera na mifumo ya uendeshaji vimeboreshwa ili kuongeza tija na ufanisi

Profesa Mwamila amesema chuo chake kitahakikisha kinachangia ipasavyo katika kufanikiwa azama ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa na uchumi wa viwanda.

No comments

Powered by Blogger.