Header Ads

header ad

GAVANA WA BENKI KUU KUWA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA SIKU YA TAKWIMU AFRIKA


Mkurugenzi wa Shughuli za Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw, Irenius Ruyobya akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika inayotarajiwa kuadhimisha tarehe 20 Novemba jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mtakwimu
Mwandamizi wa ofisi hiyo Bw. Philemon Mwenda.


……………
Na: Veronica Kazimoto,
Dar es Salaam
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yatakayofanyika  tarehe 20 Novemba, 2017 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Irenius Ruyobya amesema maadhimisho hayo yanayoratibiwa na ofisi hiyo kwa niaba ya Serikali, yana lengo la kuongeza ufahamu kuhusu nafasi na mchango wa Tasnia ya Takwimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii Barani Afrika.
Ruyobya amesema kuwa kaulimbiu ya Siku ya Takwimu Afrika kwa mwaka huu ni “Takwimu Bora za Uchumi kwa Maisha Bora”
“Kaulimbiu hii inalenga kuweka mkazo katika matumizi ya Takwimu za Uchumi kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi wote nchini na  Afrika kwa ujumla”, amebainisha Ruyobya.
Ruyobya amefafanua kuwa matumizi sahihi ya Takwimu za Uchumi yanaiwezesha Serikali kutunga sera na kutathmini programu mbalimbali kama vile Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP-II), Agenda ya Dunia ya Mwaka 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Agenda ya Afrika ya Mwaka 2063.
“Progaramu zote hizi, zina lengo la kuboresha maisha ya wananchi kwa kuhakikisha kuwa, kuna upatikanaji wa Huduma za afya, Elimu,
Miundombinu ya umeme na barabara, Mawasiliano, Utunzaji wa mazingira pamoja na Utawala bora”, amesema Ruyobya.
Jumla ya washiriki 200 kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo, Vyuo vya Elimu ya Juu, Wanafunzi wa Shule za Sekondari pamoja na Wadau mbalimbali wa takwimu nchini wanatarajiwa kuhudhuria kwenye maadhimisho hayo.
Tarehe 18 Novemba ya kila Mwaka, Tanzania huungana na nchi nyingine Barani Afrika kuadhimisha Siku ya Takwimu Afrika, kutokana na siku hii kuwa  Jumamosi, maadhimisho haya yatafanyika Jumatatu tarehe 20 Novemba, 2017

No comments

Powered by Blogger.