WASIPOKUJA NDANI YA SIKU TATU, TUNAFUNGA JENGO LA MKUKI HOUSE – DC MGANDILWA
Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Mhe Hashim Mgandilwa, leo tarehe 21/6/2017 amefanya ziara katika jengo la Mkuki House lililopo eneo la Kamata barabara ya Nyerere.
Akitoa maelezo juu ya ziara hiyo, Mkurugenzi wa manispaa ya Kigamboni ndg Stephen Katemba amesema kuwa waliamua kutembelea jengo hilo kujionea uendeshaji wake na kukutana na Waendeshaji wa jengo hilo ili waweze kueleza kwanini hawajalipa Manispaa pesa yake kwa miaka miwili mfululizo.
Awali baada ya kuwasili eneo hilo Uongozi Mzima wa kampuni inayoendesha jengo hilo walionekana kutokuwa ofisini licha ya kuwa walipewa taarifa ya ugeni huo kwa maandishi siku mbili kabla na wakaahidi kuwepo. Walipopigiwa simu na Katibu Tawala wa wilaya ya Kigamboni Bi Rahel Mhando walitoa visingizio kuwa wamepata dharula wako mbali sana na eneo hilo na hawawezi kufika.
DC Mgandilwa akiwa ameambatana na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya baada ya kupata maelezo hayo na kuona Waendeshaji walivyokwepa ugeni wake alielekeza mambo yafuatayo.
DC Mgandilwa ametoa muda wa siku tatu kwa mwekezaji huyo kufika ofisini kwake, kujieleza na kulipa pesa yote wanayodaiwa zaidi ya milioni 270 na kuwa endapo akikahidi agizo hilo hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufungwa kwa jengo hilo na kumwondoa mwekezaji huyo kwani haitakuwa na maana kuendelea kumbembeleza.
DC Mgandilwa anaendelea na ziara ya kutembelea wafanyabiashara, wawekezaji na vitega uchumi mbalimbali vilivyopo chini ya manispaa ya Kigamboni ili kujionea uendeshaji wake na kutaka kujua kama taratibu za nchi zinafuatwa ikiwemo kulipa kodi.
Post a Comment