TIC YAWAFUNDA WAJASILIAMALI
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za uwekezaji Bw. John Mnali akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo hayo leo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wajasirimali wakifuatilia mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC).
Mmoja wa wajasiriamali hao Bibi Neli William akishukuru TIC kwa kuandaa mafunzo hayo.
(Picha na Frank Shija)
………………………………………………………………..
Frank Mvungi-Maelezo
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimewataka Wajasiriamali nchini kujiamini na kutumia fursa zilizopo ili kukuza biashara zao na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uwekezaji wa TIC, Bw. John Mnali AMETOA WITO HUO wakAti wa mafunzo ya siku moja kwa wajasiriamali yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko kwa kuzingatia ubora.
Akifafanua Mnali amesema mafunzo hayo ni fursa kwa wajasiriamali wakati na wadogo kukutana na wajasiriamali wakubwa waliowekeza hapa nchini hali itakayochochea kuongeza ubora wa bidhaa na huduma wanazotoa.
“Jukumu la Kituo cha Uwekezaji hapa nchini ni kuhakikisha kuwa wajasiriamali wadogo na wakati wanazalisha bidhaa zitakazotumiwa na makampuni makubwa ya wawekezaji”, alisisitiza Mnali
Katika kuhakikisha kuwa wajasiriamali wanakuza mitaji yao Kituo cha Uwekezaji kimeshirikisha taasisi za fedha katika mafunzo hayo ili kuwapa fursa wajasiriamali wadogo na wakati kupata mikopo itakayo wawezesha kukuza uzalishaji wao.
Kwa upande wake mmoja wa wajasiriamali hao, Bi. Neli William amesema kuwa wajasiriamali Watanzania wamekuwa waoga kudhubutu kuzalisha bidhaa kwa wingi na kuzitangaza ili kukuza soko la bidhaa hizo.
“Nakishukuru Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwa mafunzo haya kwa kuwa yametujengea uwezo ambao utasaidia kukuza uzalishaji wetu na kuongeza tija”, alieleza Bi. Neli.
Aliongeza kuwa kila siku anao uwezo wa kuzalisha trei 70 za mayai hivyo baada ya mafunzo dhamira yake ni kuongeza kiwango cha uzalishaji.
Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) kimekuwa kikitoa mafunzo kwa wajasiriamali hapa nchini ili kuwajengea uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye ubora kulingana na mahitaji ya soko.
Post a Comment