TANZANIA NA AFRIKA KUSINI ZASAINI MIKATABA MITATU YA USHIRIKIANO
……………………………………………………….
Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Afrika ya Kusini zasaini mikataba mitatu ya ushirikiano katika sekta mbalimbali zitakazosaidia kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.
Hati za mikataba hiyo zimesainiwa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Marais wawili Dkt. John Magufuli na Jacob Zuma na waandishi wa habari.
Mikataba iliyosainiwa baina ya nchi hizo mbili ni hati ya muhtasari wa makubaliano ya mkutano wa tume ya pamoja ya Marais kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Afrika Kusini uliolenga kuboresha makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mkutano huo.
Hati ya makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya Bi Anuwai kati ya Serikali ya Tanzania na Afrika Kusini, inayolenga kuboresha ushirikiano katika sekta ya wanyamapori na uhifadhi.
Huku hati nyingine ikiwa ni makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya uchukuzi kati ya Serikali ya Tanzania na Afrika Kusini uliolenga kuboresha ushirikiano katika sekta ya uchukuzi.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Rais Magufuli alisema ziara ya Rais Zuma imekwenda sambamba na mkutano wa kwanza wa tume ya Marais ambapo ulibainisha baadhi ya maeneo ya makubaliano.
Rais Magufuli alisema kuwa maeneo ya makubaliano hayo yalilenga kuimarisha na kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili na njia za kundoa vikwazo vinavyokwamisha biashara baina yao.
“Hali ya biashara ya Afrika Kusini nchini kwa mwaka 2016 ni takribani Tsh Trilion 2.4 na uwekezaji wake ni Dola za Kimarekani 803.15 milioni iliyopelekea kupatikana kwa ajira kwa watanzania 20,916”alisema Rais Magufuli
Rais Magufuli alitaja maeneo mengine ya makubaliano kuwa ni kushirikiana katika sekta ya viwanda ambapo amewakaribisha wafanyabiashara kutoka nchini Afrika Kusini ili kuwekeza katika kujenga viwanda vya kusindika mazao na hivyo kukuza uchumi.
Kwa upande wa Sekta ya miundombinu na nishati wamelenga katika kuimarisha reli ya kati na upatikanaji wa umeme, ambapo Rais Dkt.Magufuli amemwomba Rais Zuma kutumia ushawishi wake katika Umoja wa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi (BRICS) ili kuisaidia Tanzania kupata mkopo kwa gharama nafuu, kwa lengo la kuendeleza ujenzi wa miradi ya reli ya kati na umeme.
Vilevile, Marais hao wamekubaliana kubadilishana uzoefu na wataalamu kupitia sekta ya utalii ikiwemo kuwakiribisha wawekezaji kutoka nchi ya Afrika Kusini kuwekeza kwa kujenga hoteli za kitalii pembezoni mwa fukwe za bahari ya Hindi.
Maeneo mengine ya makubaliano ni pamoja na sekta za madini kwa kubadilishana uzoefu na utaalamu, afya kwa kuwakaribisha wawekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kutengeneza dawa, elimu, sayansi na teknolojia ambapo Rais Zuma amekubali kupokea wataalamu wa lugha ya kiswahili watakaofundisha Afrika Kusini.
Rais Zuma alisema wataendelea kuimarisha uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na kukuza umoja wa Afrika ili kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyokabili bara hilo.
“Tumefurahi kusaini mikataba hiyo leo, pamoja na kupata taarifa ya mawaziri iliyojitosheleza katika kuainisha maeneo ya ushirikiano na utekelezaji wake itakayosaidia kuleta maendeleo katika nchi hizi mbili” alisema Rais Zuma
Rais Jacob Zuma anakamilisha ziara yake ya siku mbili leo usiku iliyolenga katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, ikiwa ni pamoja na kuanisha maeneo mapya ya ushirikiano yatakayochochea maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Post a Comment