Header Ads

header ad

KIMENUKA KIBITI,KIONGOZI MWINGINE WA CCM AUAWA KWA RISASI




unnamed
Kamanda wa polisi mkoani Pwani,kamishna msaidizi mwandamizi ,Onesmo Lyanga,wa kushoto,akizungumza jambo.(picha na Mwamvua Mwinyi).
……………………………
Na Mwamvua Mwinyi, Kibiti 

HALI ya sintofahamu bado inaendelea kutanda wilayani Kibiti ,mkoani Pwani ,baada ya kutokea mauaji mengine ya kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi ,ndani ya siku sita.
Kaimu mkuu wa wilaya ya Kibiti ,Juma Njwayo ,alieleza kwamba,mwenyekiti (CCM) tawi la Njianne ,kijiji cha Muyuyu ,ambae pia ni mjumbe wa kamati ya siasa kata ya Mtunda ,Iddi Kilungi ,ameuawa kwa kupigwa risasi.

Aidha alisema , mtoto wa marehemu Nurdin Iddi Kilungi ,amenusurika kifo baada ya kupigwa risasi ya tumbo na kutokea mgongoni.

Njwayo ,alieleza ,majeruhi alikimbizwa hospital ya mission ya Mchukwi  kwa ajili ya matibabu.

Alisema ,tukio hilo limetokea may 17 majira ya saa 1.40 usiku wakati marehemu akiwa amejipumzisha kimazungumzo nyumbani kwake .

Kaimu huyo  ambae pia ni mkuu wa wilaya ya Rufiji,Njwayo, alibainisha,watu wawili wanaodaiwa kuwa ni wauaji walifika eneo la nyumbani kwa Kilungi na kumpiga risasi na baadae kumpiga mwanae  kisha kutokomea kusikojulikana.

Alisema watu hao waliegesha pikipiki mbali ya nyumba na baada ya tukio walitokomea nayo .


Kwa mujibu wa Njwayo, amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Kibiti kumhamisha majeruhi (Nurdin Kilungi)kwenda hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi .

Alipoulizwa matukio hayo kuhusiana na masuala ya kisiasa alisema hawezi kulisemea moja kwa moja jambo hilo kwasasa.

“Siwezi kujua kama ndio chanzo ,mambo haya yanaendelea kuchunguzwa na vyombo vyetu vya kiusalama ,endapo itabainika basi umma utatangaziwa lolote lililopo lakini sio kuhisi”alisema Njwayo.

Kuhusiana na madai ya askari doria na kikosi maalum kilichopo Rufiji,Kibiti kutoingia maeneo ya vijijini ambako ndio kuna athari kubwa ,Njwayo,alieleza ,anachojua yeye ni kwamba kuna askari wanaovaa sare na wasiovaa sare ambao wanafika mijini na vijijini.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Onesmo Lyanga ,alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai ni siku sita tangu kutokea kwa mauaji mnamo may 13 mwaka huu,ambapo katibu wa CCM kata ya Bungu ,Halife Mtulia ,aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Alisema chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana kwani vyombo vya dola bado vinafanya upelelezi ili kubaini kiini halisi cha matukio hayo ya mauaji .

Kamanda huyo alisema wanaendelea kuwasaka wahusika wa matukio hayo yanayoonekana kuhusisha viongozi mbalimbali na askari polisi.

Kamanda Lyanga ,aliwataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo kwa kufichua wahalifu ambao wapo miongoni mwao pasipo kuogopa .

“Ni wazi kwamba wahalifu wanaofanya mauaji haya wana wenyeji wanaowakumbatia kwa kuwaficha hivyo yeyote atakaebainika kushirikiana na makundi ya uhalifu huo atachukuliwa hatua kali za kisheria”alisisitiza kamanda Lyanga.

No comments

Powered by Blogger.