HALMASHAURI YA WILAYA YA MISUNGWI YAWEKA MKAKATI WA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA KWA KUTOA VITAMBULISHO 12,148 KWA WAZEE
Halmashauri ya wilaya ya Misungwi imejipanga kuboresha utoaji wa huduma za Afya kwa wazee kwa kuwapatia Vitambulisho 12,148 wa wazee wa wilayani humo ili kutambulika rasmi wanapohitaji matibu.
Mkakati huo umefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo na maelekezo ya Serikali katika kuboredha huduma zitolewazo kwenye sekta ya Afya nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wazee wote wanapata matibabu bure.
Akizungumza na baadhi ya Wazee katika hospitali ya wilaya wakati akikabidhi Vitambulisho hivyo, Kaimu Katibu Tawala Peter Michael kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Misungwi, Juma Sweda, aliwataka Viongozi wa Halmashauri kuhakikisha wazee wengine waliobaki wapewe vitambulisho ili waweze kupata huduma za matibabu kikamilifu bila kubaguliwa.
Kaimu Katibu Tawala huyo, aliongeza na kusisitiza kuwa Menejimenti ya Hosipitali ya Wilaya waendelee kutoa huduma za Afya ipasavyo na kuhakikisha madawa na vifaa tiba vinapatikana wakati wote hususani kwa magonjwa mbalimbali yanayosumbua Wazee ili kulinda hazina ya wazee iliyopo nchini.
Awali akitoa taarifa ya mipango ya uboreshaji wa huduma za Afya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri hiyo, Eliurd Mwaiteleke, alisema Halmashauri imejipanga vyema na kuweka mikakati madhubuti ya utoaji wa huduma za Afya kwa ubora ambapo imeweza kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma na kuanzisha dirisha maalumu la matibabu kwa wazee kwenye Hospitali ya wilaya na Vituo vya Afya na hatimaye katika Zahanati zote, kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma za afya kwa Wazee na imeweza kufanikiwa kutoa vitambulisho kwa wazee 12,148 kati ya wazee 15,048 waliotambuliwa wilaya nzima.
Mwaiteleke alieleza na kufafanua kwamba yeye kama Mkurugenzi ameweza kutoa mwelekeo na taswira mpya kwa watumishi wote hususani sekta ya Afya kwa kuwakumbusha kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni pamoja na maadili ya taaluma zao, ili kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata mpango kazi na kutimiza malengo katika Majukumu kwa kiwango kikubwa na kuleta matokeo chanya.
Mkurugenzi huyo, alibainisha wazi kwamba baadhi ya watumishi wameanza kubadilika na kujituma zaidi na kutoa huduma kwa wananchi na uboreshaji wa miundombinu pamoja na ukarimu kwa wagonjwa na utunzaji na uandaaji wa takwimu na taarifa sahihi kwenye baadhi ya vituo vya Afya na zahanati na hali hiyo imetokana na matumizi mazuri ya mpango wa malipo kwa ufanisi (RBF) unaotekelezwa kwa sasa kwa ushindani katika kuimarisha na kuboresha miundombinu katika maeneo ya utoaji wa huduma za afya kwenye vituo husika ambapo kila kituo kilipewa Tshs. 10,000,000/= .
Amewataka Wakuu wa vituo na Zahanati zote wilayani humo kuhakikisha wanawasimamia na kufuatilia utendaji kazi wa Waganga na Wauguzi pamoja na wahudumu wote wa sekta ya afya waliochini yao, kwenye maeneo yao kutimiza malengo na kuzingatia mpango mkakati waliojiwekea na kutoa taarifa ya shughuli za utoaji wa huduma na changamoto zilizopo kwa kila robo na endapo watashindwa wajiandae kuwekwa kando.
Mwaiteleke alisema Halmashauri ya wilaya ya Misungwi inajumla ya Hospitali 1 ya Serikali, Hospitali 1 ya shirika la dini, Vituo vya Afya 4 na zahanati za kutolea huduma za Afya zipatazo 38 za serikali na 2 za binafsi zinazotoa Huduma ya kriniki, huduma ya akina mama wajawazito, huduma ya mama na mototo, huduma ya Meno, Macho , huduma ya magonjwa ya Upasuaji na Magonjwa yasiyoambukiza.
Post a Comment