WADAU wa Sekta binafsi nchini Jumanne wiki hii, wamefanya mkutano ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano wao na serikali chini ya jukwaa la Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) unaotarajiwa kufanyika Mei 6 mwaka huu.
Mkutano huo wa ndani uliandaliwa na Taasisi ya Sekta binafsi nchini – TPSF ulilenga kuwekana sawa kuhusu namna bora ya kuiwakilisha sekta binafsi katika mkutano huo muhimu, ambao Mwenyekiti wake ni Rais wa Jamhuri ya Tanzania Dr. John Pombe Magufuli.
Akiwakaribisha wadau wa Sekta Binafsi katika kikao hicho cha maandalizi Mwenyekiti wa TPSF Dk. Reginald Mengi alisema Serikali na Sekta Binafsi hawakomoani, ndio maana TPSF inahimiza wafanye kazi kwa pamoja ili kulifikisha taifa kwenye uchumi wa viwanda.
Dk Mengi pia alisema serikali na sekta binafsi wana malengo yanayofanana ya kutokomeza umaskini na kutengeneza ajira kwa wananchi, jambo ambalo linaweza kutekelezeka kwa urahisi iwapo kutakuwa na ushirikiano wa karibu baina ya serikali na Sekta Binafsi.
Katibu Mtendaji wa TNBC Mhandisi Raymond Mbilinyi alisema mkutano huo utakuwa ni fursa nzuri kwa serikali na sekta binafsi kubadilishana mawazo kuhusu wajibu wa kila upande katika kuboresha mazingira ya biashara na uzalishaji nchini ili kukuza uchumi wa nchi.
Post a Comment