INTANETI INAVYOATHIRI MAISHA YAKO YA KILA SIKU
Na Jumia Travel Tanzania
Hakuna kitu kinachoudhi kama kuwa sehemu na marafiki,
familia au ndugu lakini unakuta kila mtu ameinamia skirini ya simu yake!
Kwa kiasi kikubwa kuja kwa mtandao wa intaneti kumewafanya watu
kujikita zaidi na simu zao badala ya watu au kufaidi mazingira
yanayowazunguka.
Kuna tafiti nyingi zimekwishafanyika na kuthibitisha
kuwa muda mwingi unaotumika kwenye intaneti una madhara kama vile ya
kimwili na kiakili. Mbali na kuwepo kwa faida lukuki za mtandao huo,
Jumia Travel ingependa kukujulisha kuwa yafuatayo yanaweza kukumba
endapo utautumia vibaya:
Intaneti husababisha hali ya kujisikia vibaya, kukosa furaha na wivu. Mtu anaweza kushangaa na kujiuliza hii inaweza kutokeaje.
Jibu ni rahisi sana. Mambo tunayoyaona kwenye mitandao
ya kijamii yanayowekwa na watu maarufu, ndugu, jamaa au marafiki wa
karibu huweza kukukosesha furaha kwa namna moja ama nyingine.
Hebu jaribu kufikiria unamuona rafiki yako wa karibu
ameweka picha zake akiwa amesafiri sehemu ambayo wewe hujawahi kufika au
chakula usichowahi kukila utajisikiaje?
Ingawa sio wote wanaoweza kujisikia vibaya lakini kwa
asilimia kubwa wengi wao hupatwa na wivu au kusononeka nafsi kuona
kwamba inawezakana wao wasije kuwa na maisha kama yale.
Intaneti husababisha watu wengi kujihisi kuwa wanapitwa
na wakati. Tangu enzi za kale kila nyakati zimekuwa na mitindo tofauti
ya maisha hapa duniani. Kwa bahati mbaya sio watu wote ambao wanao uwezo
wa kuendana na mitindo au fasheni zilizopo.
Hali hii imewafanya wengi kujihisi kupitwa na wakati
endapo wasipoishi kama wanavyoona kwenye mitandao. Kupitia mitandao ya
kijamii kama vile Instagram watu wanaweza kuwashirikisha wenzao picha na
video za namna wanavyoishi kuendana na wakati. Ambapo mara nyingi yale
yanakuwa sio uhalisia wa maisha yao.
Intaneti imekuwa ni chanzo kikubwa kwa watu wengi
kutokuwa na utulivu wa akili. Nadhani hii hali inawakuta watu wengi
katika maisha yao ya kila siku katika ulimwengu wa sasa wa intaneti.
Kuna wakati unajaribu kujikita kwenye suala fulani lakini shughuli
zinazoendelea mtandaoni kupitia simu yako ni kikwazo kikubwa.
Kwa mfano, unataka kukamilisha kazi uliyopewa na bosi
wako, mara ujumbe wa Whatsapp umeingia, hujatulia Facebook, Twitter na
Instagram nazo zote zinakujulisha kuwa unapitwa huku. Kwa hali hii
sidhani kama kuna jambo ambalo mtu anaweza kulikamilisha kwa ufanisi na
usahihi unaohitajika.
Intaneti inawanyima watu fursa ya kufurahia maisha
halisi yanayowazunguka. Kwa sasa ni jambo la kawaida kabisa sasa kuona
familia imekwenda hotelini kupata chakula pamoja na kubadilisha
mazingira ya nyumbani lakini ukakuta kuanzia watoto mpaka wazazi wote
wameinamisha nyuso zao kwenye skirini za simu zao.
Hakuna tena ile hali ya zamani kwamba muda wa chakula
ndipo familia hukutana kwa pamoja, kuzungumza, kucheka na kubadilishana
mawazo juu ya yale waliyoyapitia siku nzima.
Kwa hali ilivyo sasa hivi huwezi kusikia tena vicheko au
gumzo kwenye familia nyingi kwani vyote hivyo vimeamia kwenye simu.
Usishangae ukamuona mtu anacheka mwenyewe ukadhahania ni punguani,
hapana, ni mambo ya intaneti hayo.
Intaneti imekuwa ni chanzo kikubwa cha watu kutokuwa
wabunifu katika masuala mbalimbali. Hebu jaribu kufikiria ingekuwaje
kama hizo video unazozitazama kupitia YouTube, habari unazoziona
Facebook au Twitter, au picha unazoziona kupitia Instagram; vyote hivyo
ungevipataje kama waliogundua nao wangekuwa wanatumia muda wao kwenye
intaneti kupitia kazi za wenzao.
Hii inamaanisha kwamba hatupaswi kutumia muda mwingi
kuwa watumiaji wa vitu vya kwenye intaneti badala yake nasi tuwe
wazalishaji ili kuwanufaisha na wengine zaidi.
Unaweza kukuta mtu tangu siku inaanza mpaka inaisha yeye
anaimaliza kwenye mitandao ya kijamii akipitia, kutazama na kusoma
habari za watu wengine.
Yaliyozungumzwa katika makala haya ndio maisha ya wengi
kwa sasa jinsi yalivyoathiriwa na kuja kwa intaneti. Lakini zipo mbinu
kadhaa za kuweza kujiepusha na madhila hayo yote.
Jumia Travel inashauri kwamba jukumu la mtu kuepukana na uraibu wa matumizi ya intaneti ni la kwake mwenyewe.
Kwa mfano, kujiwekea au kutenga muda maalumu wa kuingia
mtandaoni, kuzima ishara zitokanazo na mitandao ya kijamii au kuzima
kabisa intaneti kwenye simu yako mpaka muda fulani inaweza kusaidia pia.
Post a Comment