WANAWAKE WAONGOZA KWA MAAMBUKIZI YA UKIMWI NCHINI
Akizindua matokeo ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa Mwaka 2016/2017, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kwa mujibu wa utafiti huu wa mwaka 2016/17, inakadiriwa kuwa watanzania wapatao million 1.4 wanaishi na virusi vya UKIMWI na utafiti huo unaonesha kuwa kiwango cha maambukizi kwa wanawake ni asilimia 6.5 na wanaume ni asilimia 3.5.
Aidha Mh. Samia Suluhu amesisitiza kuwa kupungua kwa kiwango cha maambukizi hakumaniishi kuwa UKIMWI umeisha bali ni matokeo ya jitihada zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo wananchi katika kujilinda dhidi ya maambukizi mapya.
Awali akitoa maelezo kuhusu utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa huo ni utafiti wa nne kufanyika hapa nchini, ambapo kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 2003/04 ambao ulionesha kiwango cha maambukizi kilikuwa asilimia 7.0 na kufuatiwa na tafiti nyingine za miaka ya 2007/08 na 2011/12 iliyoonesha maabukizi ya asilimia 5.1
Amesema utafiti huu ulihusisha kaya 16,198 na kujumuisha wanakaya wote waliokuwa kwenye kaya wakilishi zilizochaguliwa na umegharimu kiasi cha Shillingi 7.4 bilioni ambazo zimetolewa na Serikali ya Marekani chini ya Mfuko wa Rais
wa Dharura wa Kupambana na UKIMWI (President’s Emergency Plan for AIDS Relief – PEPFAR).
Kwa upande wake Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu,JENISTA MHAGAMA amemuagiza mkurugenzi wa TACAIDSifikapo mwakani aweze kuanzisha kampeni itakayo wafanya wanaume kujitokeza kwa wingi katika upimaji wa ugonjwa wa UKIMWI.
Kwa mujibu wa utafiti huo mikoa ambayo kiwango cha maambukizi ya VVU ni zaidi ya asilimia 10 ni Iringa yenye maambukizi ya asilimia 11.3 na Njombe yenye asilimia 11.4 huku mikoa yote ya Tanzania Zanzibar ikiwa na maambukizi ya ukimwi ni chini ya asilimia 1.
Na James Salvatory
Post a Comment