TAMKO LA WAZIRI WA AFYA MH. UMMY MWALIMU (MB) KUHUSU UGONJWA WA KICHAA CHA MBWA
Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa ni mojawapo ya magonjwa yaliyoathiri nchi yetu na maeneo
mengi duniani. Ugonjwa huu husababishwa na virusi kutoka kwa wanyama jamii ya mbwa ambao wameathirika na virusi hivi (Mbwa, paka, mbweha, fisi na wengineo) na humwingia mwanadamu kwa kuumuuma na mate ya mnyama yenye virusi hivi huingia katika eneo lenye jeraha.
Takwimu za kidunia zinaonyesha ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa inakadiriwa kusababisha takribani vifo 59,000 ambapo kati ya hao, asilimia 36 hutokea katika bara la Afrika. Inakadiriwa kuwa kati ya 30%-50% ya waathirika wa kichaa cha mbwa ni watoto chini ya miaka kumi na tano. Pamoja na kusabisha vifo, ugonjwa huu pia unasababisha athari kubwa katika kiuchumi kwani chanjo ambayo ndio matibabu yake ni kubwa. Gharama ya chanjo inakadiriwa kuwa 150,000 kwa mgonjwa kwa bara la AfriKa, ambayo ni sawa na 6% ya mapato ya nchi katika bara hilo.
Kwa hapa Tanzania, ugonjwa wa kichaa cha mbwa uliripotiwa kwa maara ya kwanza mnamo 1932/33. Baada ya hapo, wagonjwa wameendelea kuripotiwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa viwango tofauti. Kwa mwaka huu kati ya mwezi Januari hadi Agosti, watu 17,326 wametolewa taarifa ya kuumwa na mbwa au wanyama wa jamii hiyo na kumetokea vifo 8. Takwimu hizi hazijumuishi vifo vinavyotokea nyumbani na waathirika ambao hawakufika katika vituo vya kutolea huduma za afya, hivyo tatizo hili ni linaweza pia kubwa kuliko tunavyofikiri. Utafiti uliofanyika mwaka 2002 ulibainisha kuwepo na uwezekano wa kuwepo takriban vifo 1,499 kwa mwaka nchini kutokana na ugonjwa huu.
Tafiti pia zimeonesha waathirika wakuu wa ugonjwa huu ni watoto chini ya miaka 15. Uwezekano mkubwa ni kwa sababu wao ndio wanaokuwa karibu na mbwa(anaefugwa) muda mwingi, na pia hupenda kucheza/kuchokoza mbwa wasiowafahamu njiani.
Vimelea vya kichaa cha mbwa vinapoingia katika jeraha hushambulia neva za fahamu kutoka katika eneo la jeraha, kuelekea katika uti wa mgongo na hatimae kuathiri ubongo. Dalili huanza kuonekana baada ya kuathirika kwa mfumo wa kati wa fahamu, na baadae ubongo, ambazo ni pamoja na kuwashwa sehemu ya jeraha, homa, kuumwa kichwa, maumivu ya mwili, kuogopa maji na mwanga, kutokwa mate mengi mfululizo, kuweweseka (kushtuka mara kwa mara na kuogopa), kupooza na hatimae kupoteza maisha. Wakati mwingine watu huhusisha dalili hizi na imani potofu.
Katika juhudi za kudhibiti ugonjwa huu, Tanzania ilipata ufadhili wa Bill na Melinda Gates na kushirikiana na Shirika la Afya Duniani na kuwa moja ya nchi zilizochaguliwa kutekeleza ‘Mradi wa majaribio wa Kutokomeza Kichaa cha Mbwa’ kati ya mwaka 2009-2016, nchi nyingine zikiwa ni Ufilipino na Afrika ya Kusini. Lengo kubwa la mradi huu lilikuwa ni kusaidiana na nchi hizi katika kutokomeza ugonjwa huu kwa jamii ya mbwa na paka ili wawe na virusi hivi endapo watamuuma binadamu. Utekelezaji wa mradi ulihusisha kampeni za kuchanja mbwa wote kwa mwaka mara moja. Aidha, chanjo za binadamu pia zilitolewa. Mradi huu ulitekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro Lindi na Mtwara, ambapo mbwa na paka walipatiwa chanjo kila mwaka. Katika mradi huu:
- Chanjo za binadamu dozi 28,000 zilitolewa katika eneo la mradi.
- Watumishi 101 walipata mafunzo kuhusu rabies na njia mpya ya utoaji chanjo, na jinsi ya kuhakikisha hakuna ‘kuishiwa na chanjo’.
- Mwongozo wa Kudhibiti Kichaa cha Mbwa kwa wanafunzi wa shule za msingi uliandaliwa.
- Elimu ya afya kuhusu kichaa cha mbwa na jinsi ya kujikinga ilitolewa kwa jamii kupitia kampeni za uchanjaji.
- Vielimishi jamii vilitengenezwa na kusambazwa. Kufuatia mradi huu, vifo vinavyotokana na Kichaa cha mbwa katika maeneo ya mradi vilipungua toka 17 mwaka 2010 hadi 0 mwaka 2013 hadi 2015.
Kama ilivyoelezwa hapo juu, ugonjwa huu hutoka kwa wanyama jamii ya mbwa/paka aliyeathirika na virusi hivi na kuja kwa binadamu anapomuuma. Hivyo juhudi za pamoja zinahitajika kwa sekta zote mbili ili kutokomeza ugonjwa huu.
Mambo muhimu ya kufanya ili kujikinga:
- Endapo mtu ameumwa na mbwa, hatua ya kwanza muhimu ni kuosha jeraha kwa dakika 10 au zaidi kwa maji mengi yanayotiririkika na sabuni. Kidonda kisifungwe. Kisha apelekwe haraka katika ktuo cha kutolea huduma za afya ili kupata chanjo ya kichaa cha mbwa. Ni muhimu aliyeumwa na mbwa afanyiwe tathmini ya kina katika kituo cha kutolea huduma ili aweze kupatiwa chanjo kamili na iwapo chanjo ikitolewa ni budi kumaliza kozi zote za chanjo. Wizara imekwisha kutoa maagizo kwa mikoa na wilaya kuhakikisha kuwa chanjo hizi zinanunuliwa na kutolewa kwa wananchi wanaozihitaji.
- Mtu aliyeumwa na kichaa cha mbwa awahi kituo cha kutolea huduma za afya na kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo, na ni muhimu kumaliza kozi.
- Wanyama jamii ya mbwa, paka wasiruhusiwe kulamba vidonda, kwani mate yao huweza kuleta maambukizi endapo wameathirika.
- Wamiliki wa mbwa wahakikishe wanachanja mbwa wao dhidi ya kichaa cha mbwa mara moja kila mwaka na kupata cheti.
- Mbwa wafungiwe ndani wakati wa mchana na wasiachwe kuzurura hovyo, kwani wanaweza kupata maambukizi endapo watakutana na mnyama aliyeambukizwa.
- Kuhakikisha mazingira yote ni safi, ili kutowapa chakula mbwa wanaozurura mtaani na kuzoea kuja katika mazingira tunamoishi.
- Watoto wapewe elimu na wakatazwe kuchokoza mbwa wasiowajua njiani (kuvuta mkia/masikio, kumpanda mgongoni n.k)
Katika kutekeleza mikakati na juhudi za pamoja za sekta zote zinazohusika kudhibiti ugonjwa huu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imeshirikiana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Shirika la Afya Duniani, Shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama Duniani (OIE) na asasi zisizo za kiserikali katika kuandaa ‘Mkakati wa Kudhibiti Kichaa cha Mbwa’ wenye lengo la kutokomeza ugonjwa huu ifikapo 2030.
Tunawapongeza wote wanaoshiriki kwa njia moja au nyingine katika kudhibiti kichaa cha mbwa, na tunazidi kutoa wito kwa jamii kwa ujumla kuzingatia maelekezo ya kuzuia/kujikinga na ugonjwa huu. Tunatoa shukrani kwa wadau mbalimbali wanaoshiriki nasi katika juhudi hizi- Mfuko wa Bill na Melinda Gates, Shirika la Afya Duniani, Shirika la Wanyama, Taasisi ya Afya Ifakara na wengineo.
Post a Comment