BENKI ya NMB leo imekabidhi mchango wa jezi za mpira wa miguu seti 10 pamoja na fulana 500 zikiwa na jumbe mbalimbali kuhamasisha uzingatiaji sheria na kanuni za usalama barabarani ikiwa ni kuchangia kufanikisha Tamasha kubwa la Usalama barabarani linalotarajia kufanyika uwanja wa Taifa hapo baadaye.
Msaada huo umekabidhiwa leo jijini Dar es Salaam kwa Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni na kuipongeza Benki ya NMB pamoja na wadhamini wengine kwa kujitoa kuchangia tamasha hilo la Usalama Barabarani lenye kauli mbiu “Hatutaki Ajali, Tunataka Kuishi Milele” litakalofanyika Agosti 12, 2017.
Akikabidhi msaada huo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Serikali, Omari Mtiga alisema NMB linaunga mkono usalama wa raia na mali zao na ndio maana limevutiwa kuchangia ufanikishaji wa tamasha hilo ambalo limelenga kutoa elimu kwa umma juu ya uzingatiaji wa sheria na kanuni za usalama barabarani.
Mtiga alisema NMB imekuwa mshirika mkubwa wa Jeshi la Polisi Tanzania kwani imekuwa ikishirikiana kuunga mkono juhudi mbalimbali za jeshi katika kulinda usalama wa raia na mali zao. Alisema NMB itaendelea kushirikiana na Jeshi hilo ili kuhakikisha wananchi ambao ni wateja wake wanakuwa salama salimini pamoja na mali zao.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Masauni alisema tamasha hilo lililopangwa kufanyika Uwanja wa Taifa Agosti 12, 2017 na kushirikisha michezo na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii na mapambano ya mpira wa miguu linatarajiwa kufunguliwa na Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.
Michezo itakayofanyika ni pamoja na mpira wa miguu kati ya Jeshi la Polisi na Bodaboda, Wabunge na Wasanii wa Bongo Movie na Wasanii wa Bongo Fleva. Tamasha hilo kwa ujumla litakuwa likitoa elimu ya masuala mbalimbali ya usalama barabarani lengo likiwa kupambana na ajali za barabarani.
Post a Comment