Header Ads

header ad

WAZIRI MKUU AMSIMAMISHA KAZI DED WA MBOZI

PMO_5114
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watumishi wa  Umma, Viongozi wa Dini na Viongozi wa Taasisi Binafsi wa wilaya ya Mbozi kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Vwawa wilayani Mbozi Julai 23, 2017. Kulia ni mkewe Mary na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa  Wapili  kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Limdi, Erasto Zambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
PMO_5127
Cashier wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi  Bahati Chomoka pia amesimamishwa.kazi.
PMO_5129
DT wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Simon Noeli ambaye pia amesimamishwa kazi.
PMO_5133
DED wa Mbozi, Elisey Mgoyi mmoja wa watendaji wa Halmashauri ya  Wilaya ya Mbozi ambao Waziri Mkuu aliagiza wasimashwe kazi na wafanyiwe uchunguzi na TAKUKIURU.
PMO_5191
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa jengo la Mkuu wa Mkoa wa Songwe nje kidogo ya mji wa Vwawa mkoani Songwe Julai 23, 2017. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
PMO_5264
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary  (kulia kwake) wakitazama Kimondo wakati walipotembelea Kituo cha Mambo ya Kale cha Mbozi mkoani Songwe Julai 23, 2017.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
PMO_5316
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakiwapungia wananchi wa wilaya ya Mbozi wakati walipowasili kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Kyalele wilayani humo kuhutubia mkutano wa hadhara, Julai 23, 2017. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
PMO_5356
Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakitazama nguo za batiki  wakati walipotembelea banda la wanawake wajasiriamali wa Mbozi kabla ya  mkutano wa hadahara uliohutubia wa Waziri Mkuu kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Nalyelye wilayani Mbozi, Februari 23, 2017. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa. (Picha na Ofisi a Waziri Mkuu)
……………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Bw. Eliseyi Mgoyi pamoja na maofisa wengine watatu kwa  tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.
Pia amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Songwe, Bw. Damian Sutta kuwakamata na kuanza kuwachunguza haraka maofisa hao na kisha ampelekee taarifa ofisini kwake.
Waziri Mkuu amewasimamisha kazi maofisa hao leo (Jumapili, Julai 23, 2017) wakati alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari Vwawa, akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Maofisa wengine waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Bw. Simon Noel,  Bw. Bahati Chomoka ambaye ni Cashier na Bw. Remmy Haule  ambaye ni Ofisa Ugavi.
Waziri Mkuu amesema Maofisa hao wamekiuka sheria za matengenezo ya magari ya Serikali kwa kwenda kutengeneza katika gereji ambazo hazikusajiliwa na wala hazifanyi shughuli hiyo, jambo ambalo halikubaliki.
Amesema Kampuni ya Umbwila ni moja kati ya Kampuni zinazolipwa fedha nyingi za utengenezaji wa magari ya Halmashauri ya wilaya ya Mbozi huku ikiwa haina sifa za kufanya kazi hiyo ya utengenezaji magari.Kampuni zingine ni Julius Diesel, Kasaba na Mtoni Garage.
“Mfano duka la  Umbwila ambalo linauza vipuri vya magari lakini Halmashauri inalilipa fedha kwa ajili ya utengenezaji wa magari jambo ambalo si sahihi kwa sababu lile ni duka la vipuri na si gereji. Wanamlipa muuza vipuri kama mtengeneza magari”
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “hatuwezi kuendesha Serikali kwa namna ambayo haikubaliki kwani watu tuliowapa dhamana ndio wanaongoza kwa vitendo vya rushwa na ufisadi. Wameifanya Halmashauri hii kama shamba la bibi.”
Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amemtaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mheshimiwa Eric Ambakisye kuhakikisha anasimamia vizuri utendaji ndani ya Halmashauri hiyo na kwamba Serikali inataka watu waadilifu na wenye uaminifu na nidhamu.
“Halmashauri inanuka rushwa tunataka iwe safi. Hatuwezi kukubali kuona Halmashauri hii na zingine nchini zikigeuzwa kuwa magenge. Kwa Serikali hii no, hatuhitaji rushwa wala harufu ya ufisadi.”
Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watumishi waliopewa dhamana wakijinufaisha kwa fedha za umma na kuwaacha wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za maji, afya na elimu, hivyo itaendelea kuwachukulia hatua.
Pia Waziri Mkuu amewataka Madiwani na Wakuu wa Idara katika Halmashauri zote nchini wabadilike na wahakikisha wanashirikiana na kufanya kazi kwa ushirikiano kwani wakigawanyika watashindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.

No comments

Powered by Blogger.