ZAIDI YA LITA MIL. 700 ZA MAJI KUZALISHWA
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo (wa pili kutoka kushoto) akikagua mradi wa kuchimba visima virefu 20 katika eneo la Kimbiji na Mpera Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Romanus Mwangi’ngo (katikati) akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo kuhusu utekelezaji wa mradi huo utakaowanufaisha wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na Kisarawe Mkoani Pwani wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaotarajiwa kuzalisha maji lita milioni 260 kwa siku.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Limited inayotekeleza mradi huo Bw. Mehrdad Talebi (kulia) akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo kuhusu hatua iliyofikiwa katika kutekeleza mradi huo mapema leo.
Moja ya Visima Virefu vyenye kina cha Mita 600 vikitoa maji wakati wa majaribio yaliyofanyika ili kuonesha uwezo wa visima hivyo kuzalisha maji.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo akinywa maji yanayozalishwa na visima hivyo mara baada ya kukagua mradi huo leo ikiwa ni sehemu ya ziara yake kukagua miradi ya maji inayotekelezwa na DAWASA.
……………………………………………………………………………………
Frank Mvungi – Maelezo
Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa uchimbaji Visima virefu 20 wenye thamani ya bilioni 40 katika eneo la Kimbiji na mpera vyenye kina cha mita 600 kila kimoja, vitakavyowezesha kuzalishwa kwa jumla ya lita milioni 260 za maji kwa siku.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa kila mtanzania anafikiwa na huduma ya maji safi na salama kote nchini.
“Visima vya Kimbiji na Mpera ni moja ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali kupitia DAWASA yenye lengo la kuongeza wingi wa maji katika eneo la huduma ya Mamlaka hiyo kutoka lita milioni 300 hadi kufikia zaidi ya lita milioni 700 ambazo zinajumuisha maji yanayozalishwa katika vyanzo vya Ruvu Juu na Ruvu Chini yatakayokidhi mahitaji hadi kufikia mwaka 2032.” Alisisitiza Prof. Mkumbo
Akifafanua Profesa Kitila amesema tayari visima 17 kati ya 20 vimeshachimbwa na baadhi vipo katika hatua ya upimaji wa wingi wa maji (pump testing).
“Hali ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam inaendelea kuimarika na nchini kwa ujumla lengo likiwa kuwafikia watanzania kwa zaidi ya asilimia 95,” aliongeza Prof. Mkumbo.
Aliongeza kuwa mradi huo pamoja na ile ya Ruvu Juu na Ruvu chini sasa itaondoa kabisa tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo yote yanayohudumiwa na Mamlaka hiyo ikiwemo Kigamboni, Mji mpya, Kongowe, Gongo la mboto, Pugu, Chanika, Mbagala na Mji wa Mkuranga Mkoani Pwani na maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Romanus Mwangi’ngo amesema kazi ya usanifu wa kulaza miundombinu ya kusafirishia maji imekamilika.
Mradi wa uchimbaji visima vya Kimbiji na Mpera unatekelezwa na Serikali kupitia Kampuni ya NSPT ya Iran na Serengeti ya Tanzania kwa gharama ya bilionii 40 za Tanzania ukiwa na lengo la kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam.
Post a Comment