SPORTS PESA KUSITIZA UDHAMINI WAKE KWA LIGI YA KENYA
KAMPUNI ya mashindano ya bahati nasibu ya kubashiri matokeo ya mechi, SportPesa imetangaza kwamba itasitisha udhamini wake kwa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) baada ya serikali kuidhinisha ongezeko la kodi inayolipiwa mapato na kampuni na kubashiri matokeo.
Ofisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni hiyo, Ronald Karauri amesema ongezeko hilo la kodi hadi asilimia 35 litaathiri sana biashara za kampuni hiyo.
Ofisa Mkuu wa KPL Jack Oguda amesema kwamba hatua hiyo ya SportPesa kujiondoa itakuwa pigo kubwa kwa soka la Kenya.
Aidha udhamini wa SportPesa kwa klabu za nje ya Kenya hautaathirika. Kampuni hiyo kwa sasa hudhamini klabu za Uingereza, Everton an Hull City. SportPesa ni moja ya kampuni kubwa zaidi za mashindano ya kubashiri matokeo ya mechi Afrika Mashariki.
Kodi hiyo ya juu iliidhinishwa na serikali kama moja ya njia za kuzuia watoto na vijana wa umri mdogo kujihusisha na mashindano hayo ya ubashiri wa matokeo. Wakenya waliorodheshwa kuwa miongoni mwa watu wanaoshiriki sana katika mashindano ya bahati nasibu Afrika na Kusini mwa Jangwa la Sahara na utafiti uliofanywa hivi karibuni.
Utafiti huo ulionesha theluthi mbili ya Wakenya wa kati ya miaka 17 na 35 wamewahi kushiriki. Wengi hutumia simu zao za rununu kubashiri matokeo ya ligi za nyumbani na ligi za nje, sana Ulaya.
Kumekuwepo na wasiwasi kuhusu athari ya uraibu huo kwa vijana. Wazazi na viongozi wa kidini walikuwa wameiomba serikali kcuhukua hatua.
Bunge lilikuwa awali limependekeza kodi iwe asilimia 50, lakini rais akapendekeza kodi hiyo ipunguzwe na mwishowe ikafikia asilimia 35.
Bw Karauri amesema huenda kiwango hicho cha kodi kikafifisha sekta ya kubashiri matokeo.
SportPesa pia hudhamini mashindano ya raga na ndondi Kenya. Aidha, hudhamini klabu mbili kuu za soka Kenya – Gor Mahia na AFC Leopards – pamoja na Ligi Kuu ya Kenya na Shirikisho la Soka la Kenya.
Mapema mwaka huu, ilifadhili timu ya taifa kusafiri England na kucheza dhdii ya Hull City. Kadhalika, Sportpesa wameingia na kuanza kudhamini Simba inayocheza ligi kuu Tanzania na pia timu ya taifa ya Serengeti Boys lakini Bw Karauri amesema udhamini huo hautaathiriwa.
Post a Comment