SERIKALI YATANGAZA WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA KIDATO CHA TANO MWAKA HUU
Waziri wa Nchi Ofisi Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.George Simbachawene akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu uchaguzi na upangaji wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa mwaka 2017.
Waziri wa Nchi Ofisi Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.George Simbachawene akizungumza juu ya taratibu za Uchaguzi wa Wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na Vyuo vya Ufundi kwa mwaka 2017.
……………………………….
WAZIRI wa ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene amesema Jumla ya wanafunzi 93,019 ndiyo waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo vya ufundi kwa mwaka wa masomo wa 2017.
Simbachawene ametoa taarifa hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza matokeo ya wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2016 na kufaulu kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi mwaka huu.
Alisema kuwa kati ya wanafunzi 96,018 ni wanafunzi 93,019 ndiyo wenye sifa za kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo vya ufundi kwakuwa wamefaulu vigezo vyote vya msingi.
“Kati ya wanafunzi hao 92,998 ni wa shule (School Candidates) na wanafunzi 21 walisoma chini ya taasisi ya elimu ya watu wazima”alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa jumla ya watahiniwa wa shule 349,524 wakiwemo wasichana 178,775 sawa na asilimia 51.1 na wavulana 170,749 sawa na asilimia 48.9 walifanya mtihani huo mwaka 2016.
“Watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani huo wa mwaka 2016 walikuwa 47,751 wakiwemo wasichana 24,587 sawa na asilimia 51.5 na wavulana 23,164 sawa na asilimia 48.5”alifafanua Simbachawene.
Alisema kuwa watahiniwa waliofaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu ni 96,018 sawa na asilimia 27.60 ya watahiniwa waliofanya mtihani Tanzania Bara hivyo kufanya ufaulu kuongezeka katika mwaka 2016 kwa asilimia 3.15 ukilinganishwa na mwaka 2015.
Alisema kuwa kwa mwaka 2017 uchaguzi na upangaji wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi umezingatia mwongozo wa Wizara ya elimu , Sayansi na Teknolojia wa tarehe 15 mei 2017 na hakuna fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule.
“Mwongozo huu unalenga kwamba, kigezo cha mwanafunzi kujiung na kidato cha tano na vyuo vya ufundi ni AAA hadi CCD kama cut off point kwenye masomo ya tahasusi na pili Crediti 3 na pointi zisizopungua 25 kwenye daraja, machaguo yaliyojazwa na mwanafunzi kwenye selform yake na mwisho nafasi zilizopo katika shule husika”alifafanua.
Aidha aliwataka wanafunzi wote waliochaguliwa kuripoti katika shule walizopangwa kwa wakati, endapo watachelewa kwa zaidi ya siku 14 kuanzia tarehe ya kufungua shule nafasi zao itachukuliwa na mwingine.
“Tarehe ya kuripoti katika muhula wa kwanza kwa kidato cha tabo kwa mwaka 2017 utaanza tarehe 17 july 2017 lakini kwa wanafunzi wanaoingia kidato cha sita watafungua tarehe 3 july 2017 kama ilivyokuwa imepangwa”alisema.
Hatahivyo aliwaagiza watendaji wa wilaya na mikoa pamoja na wadau wa elimu nchini kuhakikisha miundombinu ya shule ikiwemo maabara na majengo mengine muhimu yanakamilika ili yaweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano.
Post a Comment