AFRIKA MASHARIKI KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI MIUNGONI MWA NCHI WANANCHAMA
Na Immaculate Makilika.
Soko la pamoja la Afrika Mashariki linalenga kupanua na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii miongoni mwa nchi wananchama kwa maslahi yao. Hii inatoa fursa kwa raia wote na hasa Watanzania ambao wanaonekana hawafahamu ama hawatumii fursa hizo kama raia wengine wa nchi wanachama.
Ryunosuke Satoro, mwandishi maarufu wa nchini Japan aliyezaliwa mwaka 1892 aliwahi kusema “Individually, we are one drop. Together, we are an ocean” , msemo huu una maana kwamba nguvu ya mtu mmoja ni kama tone la maji na nguvu ya watu wengi ni mithili ya bahari, kwa hivyo mafanikio madhubuti hupatikana ikiwa watu watashirikiana ama kufanya kazi kwa pamoja.
Msemo huu unajibu dhima mahsusi ya chimbuko la kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa ibara ndogo ya za 76(1) na 104 (2) za Mkataba wa kuanzisha Jumuiya hii, ambayo maeneo ya msingi yaliyohusishwa katika soko hilo la pamoja ni Soko huru la bidhaa ndani ya Jumuiya, Uhuru wa raia wa Afrika Mashariki kusafiri katika nchi yoyote ndani ya Jumuiya na Uhuru wa raia wa Afrika Mashariki kufanya kazi katika nchi yoyote ndani ya Jumuiya hiyo.
Kwa uhalisia Watanzania wanaonekana ni raia wasiochangamkia fursa hizo kwa karibu ukilinganisha na raia wa nchi zingine, hii inaweza kusababishwa na kutofahamu kabisa fursa zilizoko au kuwa na uelewa mdogo. Katika makala hii mwandishi analenga anatoa elimu kwa Watanzania kuhusu fursa hizo, kwa kuweka kuelezea soko lenyewe, faida zake na maeneo ambayo Watanzania wanaweza kunufaika nayo.
Soko huru la bidhaa linasimamiwa na itifaki ya umoja wa forodha na sheria ya Afrika Mashariki ya Usimamizi wa shughuli za forodha ya mwaka 2004, ambapo kuanzia Januari mosi mwaka 2010, bidhaa zote zinazozalishwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kukidhi vigezo vya utambuzi wa uasili wake zinaweza kusafirishwa kutoka nchi moja hadi nyingine bila kutozwa ushuru wa forodha.
Ibara ya 7 ya itifaki ya soko la Afrika Mashariki inaruhusu raia yoyote wa nchi wanachama kusafiri katika nchi yoyote miongoni mwa nchi za Jumuiya na kupata ulinzi na usalama bila kubaguliwa kwa misingi ya utaifa ikiwa ni pamoja na kupata huduma za matibabu na masomo.
Aidha, raia anayetaka kunufaika na uhuru huo wa kusafiri anatakiwa kuwa na kibali maalumu kutoka vyombo husika katika kila nchi. Pia, soko hilo la pamoja linatoa uhuru wa raia wa Afrika Mashariki kufanya kazi katika nchi yoyote ndani ya Jumuiya hiyo. Lengo la uhuru huo ni kutoa fursa za ajira kwa raia wa nchi wanachama.
Raia wa nchi za Jumuiya wanatakiwa kuzingatia mfumo uliokubalika kwa kuunda soko la pamoja, ambapo kila nchi imeainisha kada zilizohusishwa na ufunguaji wa soko la ajira. Kwa msingi huo wanajumuiya wanaruhusiwa kutafuta ajira ndani ya maeneo hayo.
Kupitia makubaliano hayo, Watanzania wana nafasi ya kwenda kufanya biashara katika nchi nyingine za Jumuiya bila kuzuiwa, na hivyo kutumia fursa hiyo kusambaza biashara zao na kupata nafasi ya kubadilishana mawazo na wafanyabishara wenzao ndani ya Jumuiya.
Katika kuunga mkono ushirikiano ndani ya Jumuiya, aliyekuwa Mwenyekiti wa wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Makongoro Nyerere, alitoa wito kwa Watanzania kuchangamkia nafasi zilizopo za kufanya biashara katika nchi za Afrika Mashariki, na kwamba wananchi wajitahidi kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu soko hilo.
Watanzania wanaweza kuchangamkia fursa hizo katika sekta ya elimu, kwa nafasi ya walimu kuanzia ngazi ya shule ya msingi zinazofundisha kingereza hadi Vyuo vikuu, sekta ya kilimo, kwa nafasi ya walimu wa vyuo vya kilimo, maafisa ugani na ufundi stadi kwa ngazi ya shahada ya pili, wauguzi, wakunga na wahudumu wengine wa sekta ya Afya.
Aidha, fursa nyingine za ajira ni uhandisi wa madini, majengo, waongoza ndege na upimaji ramani.
Ili kutilia mkazo suala hilo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Msemaji wake Mindi Kasiga amesema wafanyabiashara wa Tanzania wanatakiwa kutumia fursa za biashara zinazopatikana katika soko la nchi wanachama wa Jumuiya kwa kuuza bidhaa zao ndani ya Jumuiya hiyo.
“Wafanyabiashara wanatakiwa kuchangamkia fursa ya biashara katika soko la pamoja kwa kuwa ni haki yao na ni utekelezaji wa malengo ya mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kifungu cha tano ambacho kilianzisha itifaki ya umoja wa forodha” anasisitiza Mindi.
Aidha, wizara inawataka wafanyabiashara kutoa taarifa endapo watakumbana na vikwazo visivyo vya kiforodha kupitia mfumo wa ujumbe mfupi kwa kuandika neno ‘NTB’ kwenda namba 15539, ambapo imeandaa utaratibu wa kutatua changamoto hizo.
Ni matarajio ya Jumuiya kuwa fursa hizo zinaweza kupunguza tatizo la ajira kwa kiasi kikubwa, jambo ambalo Watanzania wamekuwa wakikabiliana nalo kwa muda, kwa vile ni dhahiri kuwa Serikali haina uwezo kutoa ajira kwa kila mwenye uhitaji kwa hivyo hii ni fursa adhimu kwa watanzania kutumia ujuzi, taaluma na mitaji ili kulikabili soko hili la pamoja.
Ushiriki wa Watanzania katika soko hili utawaongezea kipato mtu mmoja mmoja, itatoa fursa ya kujifunza kutoka kwa raia wananchama wa jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kujiongezea ujuzi katika nyanja mbalimbali, sambamba na kufikia malengo ya nchi ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumu wa kati ifikapo mwaka 2025.
Post a Comment