NDUGAI AWAONGOZA WABUNGE KUPATA CHANJO YA HOMA YA MANJANO.
NA WAMJW DODOMA.
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai amewaongoza wabunge katika kupata chanjo ya homa ya manjano inayoendelea katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Akiongoza zoezi hilo Spika Ndugai amesema kuwa wabunge wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kupata chanjo hiyo ili kujilinda kupata maambukizi ya ugonjwa huo pindi wanapotembelea nchi zenye hatari ya homa ya manjano.
“Nawaomba wabunge na na watanzania kwa ujumla husasani wale wanaosafiri mara kwa mara nchi za nje kupata chanjo hii ili wawe salama pindi wanapotembelea nchi zenye hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu” alisema Spika Ndugai.
Aidha Spika Ndugai amewapongeza Wizara ya Afya kwa hatua waliyochukua kusogeza huduma ya kutoa chanjo ya homa ya manjano karibu na wabunge pamoja na mawaziri waliopo Bungeni Mjini Dodoma.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kibamba mhe. John Mnyika amesema kuwa wabunge na watanzania kwa ujumla wapate chanjo hiyo kihalali ili kuwa na kinga ya kutosha dhidi ya ugonjwa huo.
“Tuepuke ujanjaujanja wa kupata cheti cha homa ya manjano bila ya kuchanja kwani tunajitengenezea mazingira ya kuingiza ugonjwa nchini kwani kupata cheti bila ya kuchanja ni sawa unakaribisha maambukizi” alisema Mnyika.
Post a Comment