Header Ads

header ad

TAMKO KUHUSU TAARIFA YA UGONJWA WA EBOLA KATIKA NCHI JIRANI YA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO



UTANGULIZI
Ndugu Wanahabari,
Kama tulivyowatangazia kwenye taarifa yetu ya Tarehe 15/5/2017, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilipata taarifa kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
uliotangazwa na Shirika la Afya Duniani siku ya tarehe 12 Mei, 2017. Ugonjwa wa Ebola umethibitishwa kwa kupitia vipimo vya maabara na hadi tarehe 21 Mei, 2017. Idadi ya Wagonjwa imeendelea kuongezeka na kufikia 43 ambapo kati ya hao wagonjwa 4 walipoteza maisha na wengine wanaendelea kupata matibabu katika vituo mbali mbali vya kutolea huduma za afya nchini humo. Ugonjwa huu umetokea katika Jimbo la North-east Bas-Uele linalopakana na nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kukiwa na taarifa za kuenea katika maeneo mengine matano ya jirani yakiwemo Nambwa, Muma, Ngayi, Azande na Ngabatala. Wengi wao wamekuwa na dalili za Homa, Kutapika na Kuharisha Damu pia kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili.
Wizara ya Afya ya Kongo ikishirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) imeendelea kutekeleza mikakati ya udhibiti wa ugonjwa huu nchini Kongo, ikiwa ni pamoja na kuanzisha maabara ya upimaji wa ugonjwa huo katika wilaya ya Likati ili kuweza kutambua ugonjwa huu mapema.
Aidha, Shirika la Afya Duniani limefanya tathmini ya uwezekano wa ugonjwa huu kusambaa nje ya eneo hilo, na tathmini hii imeonesha kuwa kuna uwezekano mdogo wa ugonjwa huu kusambaa nchi jirani kwa kuwa tayari Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo pamoja na Shirika la Afya Duniani wanaendelea na mikakati ya kudhibiti ugonwa huo.
Hatua zilizochukuliwa hadi sasa na Wizara kufuatia kupatikana kwa taarifa ya Ugonjwa huu huko DRC ingawa hakuna mgonjwa yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola hapa nchini hadi wakati huu, nchi yetu inapakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,hata hivyo kuna uwezekano wa ugonjwa huu kuingia hapa nchini kutokana na mwingiliano  wa watu, hasa wasafiri wanaotoka na kuingia hapa nchini. Kutokana na hali hii wizara inaendelea kuchukua tahadhari ili kuzuia ugonjwa huu usiingie hapa nchini. Hivyo, hadi sasa Wizara imefanya yafuatayo,

Kupitia tamko la WAMJW la tarehe 15/5/2017, Wizara imetoa tahadhari ya ugonjwa huu kwa wananchi katika Mikoa yote na hasa ile inayopakana na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambayo ina maingiliano ya karibu nan chi ya DRC.Mikoa hiyo ni kama ifuatayo; Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya na Songwe.
Kutoa taarifa rasmi kupitia kwa Makatibu Tawala na Waganga Wakuu wote wa Mikoa kupitia OR-TAMISEMI na kuzitaka Mamlaka husika kutoa tahadhari ya ugonjwa huu na kuweka mikakati thabiti ya udhibiti magonjwa.

Kuitisha mkutano wa dharura wa kikosi kazi cha Taifa (National Task Force) kikao cha kwanza kilifanyika mnamo tarehe 15 Mei 2017 na kutoa maamuzi mbalimbali ambayo yanayofanyiwa utekelezaji hadi sasa. Aidha vikao hivi vinaendelea kufanyika kila wiki, ili kuweza kufanya tathmini ya mikakati tuliyojiwekea kulingana na taarifa zinazotolewa na Shirika la Afya Duniani kila siku za hali ya ugonjwa huo unavyoendelea nchini Kongo.

Timu za Wataalamu kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI zimekwenda katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya na Songwe. Timu hizi zimeshirikiana na Timu za Mikoa husika kupanga mikakati ya namna ya kudhibiti ugonjwa huu. Aidha timu hizi pia zimekwenda vituo vya mipakani kuimarisha mikakati ya udhibiti wa wasafiri watokao Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo
Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa Integrated Disease Surveillance and Response ambapo kwa sasa mafunzo yanaendelea Mkoani Rukwa na wafanyakazi 238 wanaendelea kupatiwa mafunzo. Mafunzo haya yatafanyika pia katika mikoa yote inayopakana na nchi jirani ya Jamhuri ya Kongo

Vile vile Vituo vya mipakani (Points of Entry) vimepatiwa vifaa kinga ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, ambako ndani yake kuna gauni la kujikinga, miwani (google), na Buti (Boots). Aidha ugawaji wa vidonge vya klorini umefanyika pia  kwa ajili ya kuzuia maambukizi kwa wafanyakazi wa afya (Infection, Prevention and Control measures) Ugawaji ulifanyika katika Mikoa ya Mbeya (Tunduma), Songwe Airport, Kilimanjaro ( KIA , Horohoro, Holili, Tarakea, Kagera (Kabanga, Rusumo, Murongo, Mutukula) Kigoma (Sea Port, Air Port, Manyovu, Mabamba) Mwanza Airport. Pamoja na Vifaa vilivyo pelekwa mipakani, Wizara imepeleka  seti 100 za vifaa kinga vya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Ebola  katika kila  MSD zones ( Mwanza, Tabora, Moshi, Mbeya)

Kuimarisha mfumo wa kielektroniki wa Ugavi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba katika mikoa iliyoko kwenye mpaka wa Jamhuri ya Kongo  ili kurahisisha na kusogeza huduma hiyo kwa ukaribu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya

Kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji katika vituo vya mipakani ikiwemo viwanja vya ndege na mipaka ya nchi kavu na bandari katika mikoa inayopakana na Jamhuri ya Kongo ikiwemo vituo vya; Rusumo, Kabanga, Mtukula, na Bandari ya Kigoma juu ya utambuzi na utoaji taarifa kwa haraka. Hatua hizo ni pamoja na;

Kuanzisha ukaguzi ikiwemo upimaji wa joto la mwili (Thermal Screening) kwa wasafiri wanaotoka au kupitia Jamhuri ya Kongo. Hii ni pamoja na kuagiza  mashine 4 za nyongeza kwa ajili ya  Thermal Screening kwa mipaka ya Horohoro,Mutukula, Rusumo na Sirari ili kuimarisha ufuatiliaji huu. Hadi sasa kuna jumla ya Thermal Scanner 11 na baadhi zipo kwenye matengenezo katika Point of Entries (Songwe Airport, Tunduma, Namanga, Tarakea, Kabanga, Murongo, Kigoma sea port, Kigoma Airport, Manyovu, Mabamba, Mwanza Airport na JNIA)

Kuanzisha rejesta ya kurekodi wasafiri ambao watakuwa wametoka katika Jamhuri ya Kongo ili kuweza kuwafuatilia kwa karibu iwapo watapata dalili za ugonjwa huu. Aidha Pamoja na rejesta, wasafiri watakaotoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo watapaswa kujaza fomu maalamu ili kuweza kupata taarifa zao na ili kurahisisha ufuatiliaji wa wasafiri hawa iwapo wataonesha dalili za ugonjwa huu

Kuendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia mabango, vipeperushi, Radio, Televisheni na mitandao ya kijamii. Elimu ya ugonjwa huu inatolewa pia kwa njia ya kupiga simu kwenda namba 117. Huduma hii inatolewa bila malipo kwa mitandao yote.

Wizara inaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Shirika la Afya Duniani (WHO), US-CDC pamoja na mashirika mengine ya Kimataifa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu  za Kimataifa na Kitaifa. Kwa sasa Wizara inapokea taarifa ya kila siku ya Ugonjwa wa Ebola, na kuzifanyia tathmini kwa karibu na kutoa maelekezo kwa Maofisa Mbalimbali wakiwemo Waganga wakuu wa Mikoa ili kuona jinsi hali inavyoendelea na kuboresha mipango yetu.

Hitimisho
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu na waendelee kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu. Aidha Wizara inaendelea kusistiza kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huu hapa nchini.

Vilevile, Wizara inaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali katika kuimarisha ufuatiliaji na kutekeleza mikakati ya kudhibiti ugonjwa huu ili usiingie hapa nchini. Pia Wizara itaendelea kutoa taarifa pamoja na Elimu ya Afya kwa Jamii kadri itakavyohitajika.

AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA

No comments

Powered by Blogger.