Header Ads

header ad

PLAN INTERNATIONAL YAWAWEZESHA VIJANA 7300 KATIKA MIKOA MITANO


Image result for nembo ya plan international



Shirika lisilokua la Kiserikali la Plan International limewawezesha jumla ya vijana 7356 wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwapatia mafunzo ya Ufundi na Stadi za maisha ili waweze kujiajiri au kuajiriwa.

Takwimu hizo zimebainishwa na Meneja wa Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE), Simon Ndembeka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu idadi ya vijana waliopangwa kufikiwa na mradi huo wa miaka mitatu unaotegemewa kuisha mwaka 2018.
Ndembeka amesema kuwa mradi huo wa miaka mitatu ulioanza tangu mwaka 2015, unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA, UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) na umepanga kuwafikia kwa awamu jumla ya vijana 9100.

“Mradi huu umepanga kuwafikia vijana 9100, kati yao wasichana ni asilimia 53, wavulana asilimia 37 pamoja na asilimia 10 kwa ajili ya vijana wenye ulemavu hivyo mpaka sasa mradi unavyokaribia ukingoni tumeweza kuwafikia vijana 7356, tunaamini tutawafikia vijana wote waliopangwa na mradi ifikapo mwaka 2018,” alisema Ndembeka.

Ameongeza kuwa mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa kwani umewawezesha vijana wengi kujikomboa kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi kutokana na fani walizozisomea chini ya mradi hasa wasichana kwani wengi wao wamekuwa wakipewa mimba na baadae kutelekezwa wakiwa hawana mahali pa kutegemea.

Kwa upande mwingine, Ndembeka amesema kwa sasa jamii imetambua kuwa vijana wenye ulemavu wanaweza wakafanya jambo kama wakiaminiwa na kuwezeshwa hivyo shirika limepata mafanikio katika kuwawezesha vijana wenye ulemavu ili waweze kujitegemea na kuwasaidia wengine.

Meneja huyo amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni upatikanaji wa vijana wenye ulemavu kwa sababu sio jamii nzima inaelewa kuwa walemavu wanaweza wakafanya kazi hivyo wanaamua kuwaficha ndani tabia ambayo inatakiwa kukomeshwa kwa nguvu zote.
Powered by Blogger.